
Vidic naye adaiwa kuaga Manchester United
Beki wa kushoto aliyepata kudaiwa kuwa bora zaidi duniani, Ashley Cole anakaribia kuondoka Chelsea.
Mchezaji huyo aliyeichezea England mechi 98 tayari anawindwa na klabu tatu kubwa.
Mkataba wa Cole unaisha mwisho wa msimu huu, ambapo inadaiwa kwamba
amepewa ofa ya mkataba wa mwaka mmoja tu asioutaka, kama ilivyokuwa kwa
Didier Drogba.
Sera ya Chelsea imekuwa kwamba hakuna kutoa mkataba wa zaidi ya
mwaka kwa wachezaji wenye umri wa zaidi ya miaka 30, na Cole anayo 31.
Habari hizi zinakuja wakati beki huyo akiomba huruma ya Chama cha
Soka (FA) England baada ya kuwatukana maofisa wake kwa kutumia mtandao
jamii.
Cole alikasirishwa na jinsi FA kubeza utetezi wake kwa John Terry
aliyemtusi kibaguzi Antony Ferdinand wa Queen Park Rangers (QPR). FA
ilisema Cole ni mwongo na ushahidi wa Terry ulikuwa wa kutunga.
Wakati safari ya Cole ikikaribia ukingoni Stamford Bridge kama
Drogba anayecheza China, makocha wake wa zamani, Jose Mournho wa Real
Madrid na Carlo Ancelotti wa Paris Saint-Germain wanadaiwa kusubiri
kumchukua.
Ni Ancelotti aliyetangaza hivi karibuni kwamba Cole ndiye beki bora
zaidi wa kushoto, na kwamba klabu inayotaka uimara lazima imtafute.
Hata hivyo, si ajabu Cole asiondoke kwenye Ligi Kuu, kwani Kocha
Mkuu wa Manchester United, Alex Ferguson anadaiwa kumtaka Cole siku
nyingi.
Kama alivyomnyakua Robin Van Persie wa Arsenal mkataba wake
ulipokaribia kumalizika Emirates, Ferguson anaelekea kunyatia mazingira
ya Chelsea na Cole ili Januari aingie Old Trafford.
Lakini, kwa upande mwingine inadaiwa kwamba Cole anatikisa tu
kiberiti wala hana mpango wa kuondoka, bali ni namna ya kupata mkataba
mrefu au fedha nyingi zaidi Stamford Bridge.
Watu wa karibu naye wanasema kwamba Chelsea wanatakiwa kuonesha
heshima kwa Cole kwa mchango aliotoa kwa timu hadi kutwaa kombe la
Ulaya, kwani umri haujamzuia kucheza vyema.
Iwapo Cole ataamua kuondoka Chelsea kwa sababu zozote, kuna
uwezekano wa nafasi yake kuchukuliwa na Benoît Assou-Ekotto wa Tottenham
Hotspurs.
Taarifa zaidi kuhusu kuhama wachezaji zinamgusa nahodha wa
Mashetani Wekundu, Nemnaja Vidic anayehusishwa na kuhamia klabu ya
Kirusi inayomwaga noti, Anzhi Makhachkala, inayotaka kumpa mshahara wa
Pauni milioni 12 kwa mwaka baada ya kodi.
Hata hivyo, si rahisi kwa Ferguson na United kwa ujumla kumwacha
beki huyo wa Serbia aliyerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda
mrefu aondoke, kwani ni nguzo kubwa ya safu yao ya ulinzi.
No comments:
Post a Comment