*Wachezaji wana raha, wamejipanga upya
Robin Van Persie ameanza kusahaulika Arsenal, baada ya kuondoka
majira ya kiangazi na kujiunga na Manchester United kwa dau la pauni
milioni 24.
RVP aliondoka akiwa na hasira fulani na kukosa shukurani kwa
waliomfikisha kileleni kisoka, akidai klabu imeshindwa kuweka sera
madhubuti za kuleta vikombe Emirates.
RVP amefunga jumla ya magoli 96 katika mechi 200 za ligi, ambapo msimu uliopita ndio alikuwa bora zaidi, akifunga magoli 30.
Ameshaondoka na sasa anachezea Mashetani Wekundu, na wadau wa
Arsenal hawakuchelewa kupiga hesabu za faida za muda mfupi na mrefu za
kumuuza Mdachi huyo.
Klabu Imepata Fedha Nyingi
Kitita cha pauni milioni 24 ilikuwa fedha nzuri kwa mchezaji ambaye
umri wake unakwenda, aliyekuwa amebakisha msimu mmoja tu kwenye mkataba
na aliyekwishatamka hataki kubaki klabuni.
Arsenal wangeweza kumbakisha kwa nguvu hadi msimu uishe, lakini
hangecheza kama alivyokuwa, na mbaya zaidi angeondoka bila klabu kupata
senti tano muda wake ukaisha.
Amani Inajengeka na Kudumu Klabuni

Itakumbukwa kwamba, Robin hakuwa akipenda mchezaji mwingine mwenye
uwezo kumshinda, na hata lawama zake kwamba klabu hainunui wachezaji
hazikuwa za dhati.
Robin anajulikana wazi kwamba hakufurahia jinsi wachezaji wa aina
ya Aaron Ramsey walivyokuwa wakipanda chati klabuni hapo, hadi Ramsey
akaja kuvunjwa mguu na mlinzi wa Stoke City, Ryan Shawcross; sasa Ramsey
amerejea na anachanua.
Baada ya Ramsey kuumia, Wenger hakusajili mchezaji kwenye namba
hiyo, lakini Robin aliendelea kujiona kama mfalme na kutotaka yeyote
amfikie.
Hata alipoanza ngebe za kuondoka, inasemwa hakufurahishwa na
kusajiliwa kwa Podolski, mtu ambaye ni wazi ni msaada kwa klabu na timu.
RVP angebaki, wachezaji wenzake ambao walishajua tabia yake
wangejihisi vibaya, kwamba yupo klabuni tu kwa sababu anatakiwa wala
hachezi kwa kujituma.
Hali hiyo ingeweza kusababisha akabaki anasononeka muda wote, na
timu ingepata hasara. Ni bahati mbaya amekwenda kwa mahasimu wa Arsenal
kisoka, lakini pesa tamu.
Kuondoka kwa RVP kunafungua mwanya kwa kizazi kipya cha washinda
mechi kujitokeza na kujipanga, maana watu wa nje walikuwa wakidai kila
wanaposhinda kwamba Arsenal wanabebwa na RVP.
Kukosekana kwake kunawafanya wengine wajitokeze kuchangia mabao na ushindi kwa timu.
Wapo akina Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain, Lukas Podolski, Gervinho na Santi Cazorla.
Olivier Giroud ameanza mambo yake, lakini pia kuna kinda la miaka
17, Serge Gnabry aliyejumuishwa kwenye kikosi cha ligi ya mabingwa
Ulaya.
Kuondoka kwake kumetupilia mbali mtanziko uliokuwapo kwa wengi juu
ya hatima yake, au kwamba Arsenal haingeweza kusimama bila yeye,
akifuata msururu wa nyota walioondoka kabla yake, japo wengine waliaga
kwa heshima bila dharau.
Ukweli leo hii ni kwamba Arsenal wanajiona hawatetereki hata
aondoke nani. Hakuna tena kigugumizi kama kilichotanda wakati RVP
akitikisa kibiriti. Sasa timu inajisuka vyema, imeanza vizuri ligi
japokuwa bado kuna maeneo ya kurekebisha.

Donge nono lililopatikana kwa kumuuza RVP linaweza kuwekezwa kwa
kununua wachezaji wanaohitajika, maana Kocha Arsene Wengere amekuwa
akishutumiwa wakati mwingine kwamba hatumii fedha.
Lakini usajili wa Cazorla anayesemwa kuziba kabisa pengo la Cesc
Fabregas na pia kununuliwa kwa Lukas Podolski na Giroud kunaonesha
Wenger yu tayari kutumia fedha akiona inafaa.
Uuzaji wa RVP ulitokea baada ya watatu hao kusajiliwa, kwa hiyo
bosi wa Washika Bunduki wa London ana fedha kibindoni kwa ajili ya
kuimarisha kikosi Januari au hata kiangazi kijacho.
Pauni milioni 20 zinaweza kununua chipukizi kadhaa au mchezaji mmoja sampuli ya Cazorla.
Nahodha Mpya Ataleta Mambo Mapya
Kuondoka kwa Robin kunafungua mwanya kwa nahodha mpya kuleta
utambulisho tofauti klabuni, badala ya uhafidhina ule ule wa zamani.
Licha ya tabia yake ya kutotaka wengine kumfikia kisoka, japo wanampita, kama nahodha yalihitajika mabadiliko.
Leo yupo Thomas Vermaelen, na kawaida ni kwamba manahodha wote
huongoza kwa mifano yao wenyewe. RVP alifanya hivyo kwa kufunga mabao,
Vermaelen anakuja kivingine na kujenga timu bora zaidi ya ushindi.
Wakati kama huu mwaka jana, Arsenal walikuwa wameshachakazwa vibaya
sana, kwa wingi wa magoli na mechi walizoshindwa kwenye ligi, tofauti
na sasa ambapo wamepoteza kwa tabu mechi moja dhidi ya Chelsea.
Ndiyo maana inasemwa RVP alikuwa akidaiwa kuwabeba Arsenal – katika
njia sahihi au potofu. Sasa yupo kepteni mpya, mwenye moyo, dhamira, ni
msemaji na ana uzoefu, pasipo upungufu wa kiwango cha teknolojia, basi
sura mpya ya Arsenal inachanua.
Ni kweli kwamba kunyanyua kombe kwa timu iliyotoka patupu kwa miaka
minane kingekuwa kipindi kizuri mno cha mpito kwa Mbelgiji huyu.
Hata hivyo, inatosha tu kwa sasa kwamba timu inakwenda vizuri, na
yeye anazo sifa za kuwa kwenye nafasi hiyo, wenzake wakimuunga mkono.
No comments:
Post a Comment