
Liverpool yachipua, Arsenal waoga kichapo
Marejeo ya Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya mapumziko yamekuja na wimbi la ushindi kwa baadhi ya vigogo wa ligi hiyo.
Licha ya kuanza kujifunga, Manchester United walifanikiwa kusawazisha makosa yao na kuwachapa Stoke City mabao 4-2.
Majirani zao wamwaga fedha, Manchester City, wakicheza watu 10
walifanikiwa kukwepa kipigo kwa West Bromwich Albion kwa kusawazisha na
kushinda 2-1.
Vinara wa ligi hiyo, Chelsea waliendelea kutoa dozi, nao wakitoka
kwenye mbinyo wa mabao 2-1 hadi kushinda kwa 4-2 nyumbani kwa Tottenham
Hotspur na kujitanua kileleni mwa ligi.
Arsenal waliwashangaza wengi kwa kukubali kichapo cha bao 1-0
walipocheza nyumbani kwa Norwich City ambao tangu kuanza ligi
hawajafanya vyema.
Lakini wana Anfield, Liverpool walikuwa na la kujivunia, baada ya kupata ushindi wa kwanza wa ligi nyumbani.
Lilikuwa bao la chipukizi Raheem Sterling anayeanza kujihakikishia
namba katika kikosi cha kwanza, lililoondoa mkosi kwa Wekundu hao kwa
kuwakandika Reading bao 1-0.
Wigan wameendelea na matatizo yao kwa kukandikwa mabao 2-1 na
vijana wa Swansea waliokuwa wameanza kusinzia baada ya kuanza vyema
msimu huu.
Ufufuko wa Southampton kwa upande mwingine, ulionekana kuwa geresha
tu, pale walipokubali kisago cha mabao 4-1 kutoka kwa West Ham United
ya Sam Allardyice.
Utata wa Aston Villa uliendelea, baada ya kuadhiriwa kwa kufungwa bao 1-0 na Fulham katika mzunguko huu wa nane wa EPL.
Edin Dzeko alikuwa shujaa wa mabingwa watetezi, Manchester City,
kwani aliingia na kupachika mabao mawili katika dakika za mwisho mwisho
na kuwanusuru City kupata kichapo cha kwanza cha ligi.
City walijikuta katika wakati mgumu baada ya James Milner kupata
kadi nyekundu mapema, ikiwa ni ya kwanza tangu aanze kucheza soka,
kutokana na rafu mbaya dhidi ya mshambuliaji wa West Brom,
Shane Long aliyekuwa anakwenda kufunga.

Wayne Rooney alijifunga mwenyewe kabla ya kuifungia Manchester
United mabao mawili katika ushindi dhidi ya Stoke uwanjani Old Trafford.
Wengine waliofunga kwa United ni Robin Van Persie na Danny Welbeck.
Chelsea walibadili mchezo kwa mabao mawili ya haraka haraka ya Juan
Mata yaliyofanya matokeo yasomeke 3-2 kabla ya Daniel Sturridge kuingia
dakika za mwisho na kufunga bao la nne.
Andre Villas-Boas alitumia kila silaha aliyokuwa nayo kuwaadhibu mahasimu waliomfukuza kazi Machi mwaka jana.
Hata hivyo, alichopata ni mabao mawili tu kutoka kwa beki William Gallas na Jermain Defoe.
Kichapo cha Arsenal ni cha pili msimu huu, tena katika mechi tatu
tu, safari hii ikiwa mikononi mwa Norwich ambao ni ushindi wa kwanza.
Ajabu ni kwamba Norwich walipachika bao dakika ya 19 tu ya mchezo
kupitia kwa Grant Holt, na Gunners wakashindwa kulikomboa, licha ya
kucheza kikosi kamili.
Kocha Brendan Rodgers wa Liverpool alikuwa katika bahari ya
majaribu tena, kwani alikuwa akikabiliana na timu aliyoifundisha siku
zilizopita.
Sterling anayechezea pia timu ya taifa alimng’arisha kwa kupachika
bao kutokana na pasi nzuri ya mshambuliaji mwandamizi pekee aliyebaki
kikosini, Luis Suarez.
Sterling anaweka historia ya kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi
wa Liverpool baada ya Michael Owen. Sterling ana umri wa miaka 17 na ana
asili ya Jamaica, japokuwa ameamua kuchezea timu ya taifa ya England.
No comments:
Post a Comment