Wachezaji wamewatolea uvivu viongozi wao
Swansea, Wigan wagomea fulana za kampeni
Rio, Roberts, Pienaar, Cisse, Lescott vinara
Sakata la ubaguzi wa rangi kwenye soka limeingia hatua mpya, baada ya wachezaji kadhaa weusi kuwatolea uvivu wanafiki.
Mshambuliaji wa Reading, Jason Roberts, Mwingereza mwenye asili ya
Grenada alivunja ukimya kwa kukataa kuvaa fulana inayoashiria upigaji
vita ubaguzi huo.
Aliungwa mkono na wachezaji zaidi ya 30, akiwamo Rio Ferdinand wa
Manchester United, wanaoamini kwamba taasisi ya Kick It Out haijachukua
hatua stahili kuukabili ubaguzi. Imekuwa utamaduni kila Oktoba
kuadhimishwa wiki ya kupinga ubaguzi, na wachezaji wote walitarajiwa
kuvaa fulana hizo kwa wiki moja kuanzia Oktoba 18.
Matukio haya yamekuja baada ya John Terry wa Chelsea kumbagua Anton
Ferdinand (mdogowe Rio anayechezea Queen Park Rangers – QPR) na Luis
Suarez wa Liverpool kumtolea lugha ya aina hiyo Patrice Evra wa United,
kisha kukataa kumpa mkono mara mbili.
wachezaji waliokataa kuvaa fulana hizo kabla ya mechi za mwisho wa
wiki ni Victor Anichebe, Sylvain Distin na Steven Pienaar wa Everton
waliokuwa wakipambana na QPR.
Wenyeji wao, yaani QPR waliokataa fulana hizo ni
Anton Ferdinand kama alivyotarajiwa, Djibril Cisse, Shaun Wright-Phillips, Nedum Onouha na Junior Hoilett.
Jumamosi wachezaji wengi zaidi waligombea fulana hizo, nao ni Micah
Richards na Joleon Lescott wa Manchester City na Rio Ferdinand wa
Manchester United.
Mwassi wa mgomo huo alitimiza azma yake katika uwanja wa Anfield,
naye ni Jason Roberts wa Reading wakati Kenwyne Jones wa Stoke naye
aliitupa mbali fulana hiyo.
Swansea na Wigan walionesha mshikamano wa ajabu kwani wachezaji wao wote hawakuvaa fulana hizo.
Hatua ya wachezaji hao kukacha fulana zenye nembo yenye maneno ya
Kiingereza; ‘Mchezo Mmoja Jamii Moja’ imekuja baada ya Ashley Cole wa
Chelsea pia kumtetea mshirika wake Terry kortini.
Cole ambaye ni mweusi aliku kubezwa na Chama cha Soka (FA) cha
Uingereza kwa vile ushahidi wakeu ulikuwa wa uongo, naye akajibu kwa
kuwatusi maofisa wa FA.
Matokeo ya hatua yake ya kiburi na majigambo imeishia kutozwa faini
ya Pauni 90,000. Rio amemfananisha Cole na ‘choc ice’, yaani barafu
ambayo nje huweza kuwa nyeupe na ndani nyeusi. Rio alipigwa faini ya
Pauni 45,000.
Terry aliadhibiwa kulipa faini ya Pauni 220,000 na kukosa mechi nne za ligi, akadai angekata rufaa.
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita amesema hatakata rufaa,
hatua inayoonesha ameridhia adhabu zote na anajua kwamba alifanya makosa
ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Anton.
FA ilimwadhibu Suarez kukosa mechi nane na kulipa faini ya Pauni
40,000 kwa makosa yake ya kujirudia rudia. Chelsea nao wamemwongezea
Terry adhabu na walisema Cole naye angeadhibiwa, lakini Terry anabaki
nahodha wa mabingwa hao wa Ulaya.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, taasisi ya Kick It Out
inachukuliwa na wachezaji weusi kwamba imelemaa na haijakuwa makini
kushughulikia tatizo hilo, hivyo wakaamua kuachana na fulana zao, ili
walau kufikisha ujumbe.
Wakati makocha wa timu ambazo wachezaji wao waligomea fulana hizo
wakionesha upole, Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson aligeuka
mbogo, akidai Rio angeshughulikiwa.
Lakini ni Rio huyo huyo anayetegemewa na klabu yake katika ulinzi Jumanne hii katika hatua za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Jumatatu asubuhi, Rio na Ferguson walionekana mazoezini, wote wakitabasamu na kujenga hisia kwamba hapangekuwa na adhabu yoyote.
Yalichapishwa madai mwishoni mwa wiki, kwamba huenda Rio
angeadhibiwa kwa kukatwa mshahara wa wiki mbili, ambao ni Pauni 220,000,
na hatima yake Man U kuwa shakani. Si rahis kwa kocha Ferguson kuchukua
hatua kama hiyo.
Hata angeadhibiwa Rio ni mtu wa msimamo na katika masahibu ya mdogo
wake na mengine ya wanaodhalilishwa, amekuwa nao siku zote, bila
kuogopa kitakachompata.
Pengine ni kwa sababu hiyo, Ferguson amekengeuka na kusema kwamba
hakuna tatizo kati yake na Rio na kwamba mambo yote yameshawekwa sawa.
Akizunguza na waandishi wa habari Jumatatu alasiri, Ferguson
alisema kwamba kilichotokea ni ukosefu wa mawasiliano kutoka kwa Rio,
aliyetarajiwa kutoa notisi ya kusudio la kutovaa fulana hiyo.
Ferguson alionekana kuudhika, hasa kwa sababu alikuwa amemshambulia
Roberts wa Reading kwa kutangaza kugomea uvaaji fulana, akisema kwamba
mshambuliaji huyo hakuwa na hoja.
‘Kick Racism out of Football’ ilianza mwaka 1993 kabla haijabadilika na kuwa ‘Kick It Out’ mwaka 1997.
Katika msimu wa mwaka 2010/11 taasisi hiyo ilikuwa na bajeti ya
£453,913. Kati ya hizo, £330,000 zilitolewa na FA, taasisi inayoendesha
Ligi Kuu na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA).
Akizungumzia suala la ubaguzi kwenye soka, Mark Hughes – Kocha Mkuu
wa QPR anayochezea Anton Ferdinand anasema itachukua muda mrefu
kumaliza tatizo hilo.
Kocha wa Everton, David Moyes anawaunga mkono wachezaji wake watatu
kwa walilofanya, japokuwa anasema kwamba hiyo haina maana anakubaliana
na hoja yao.
Ni vigumu kwa kocha yeyote mweledi kuwaadhibu wachezaji weusi kwa
sababu eti wamekataa kuvaa fulana hizo, kwa sababu wapo wanaowatukana
mara nyingi wasioadhibiwa. Itachukua muda kupata suluhu katika hili.